Tuesday, September 2, 2008

NI NINI RUIA, AZMA NA MAADILI YA NCHI INAYOITWA TANZANIA?

KATIKA Mpango wa Kimkakati [Strategic Plan] kwa kawaida taasisi huwa inaangalia pale ilipo na kule inakotaka kwenda na kuwepo baada ya miaka kadhaa!

Hii ni determination ya kile kitu tunachokiita VISION, MISSION AND VALUES FOR THE ORGANIZATION OR INSTITUTION OR COUNTRY na kwa leo hapa ni hii nchi inayoitwa TANZANIA!

Swali la kujiuliza hivi Tanzania inaisheshimu Vision iliyojiwekea yenyewe sikumbuki tarehe lakini ninaamini wakina kaka Mwapachu na wenzake walifanya kazi nzuri tu, japo kwa leo kuna mambo yanaweza kuwa yamepitwa na wakati! Au yanastahili kuongezwa mengineyo kutokana na kasi ya mabadiliko inayosababishwa na hali ya kiuchumi ya dunia, utandawazi na teknolojia!

Baada ya kuwa na VISHENI hiyo sasa wanasiasa wanatuambia nini kuhusu nini visheni ndogo na wizara na MISSION au AZMA za wizara na mikoa mbalimbali na viongozi mbalimbali wa kijamii na kiuchumi!

Na je kwa utamaduni, maadili yasiyo maadili na tabia zetu hizi zinazoitwa za Kiswahili tunaweza kutekeleza visheni na azma hizo?

Mimi ninaamini bila kuwa na maadili ya Kitanzania yanayojulikana na kuheshimika ulimwenguni kote basi itakuwa ni shida sana kutekeleza kazi iliyo mbele yetu.

Ni lazima Watanzania tuzungumze. Tuzungumze tunastahili sisi na vizazi vyetu kuwa ni watu wa namna gani?

Je, tunastahili kuheshimu na kuhifadhi tamaduni na lugha za makabila yetu ya asili na kuifanya lugha ya Kiswahili ndio utamaduni na lugha peke?

Je, tunastahili kujifunza lugha nyinginezo? Ni lugha zipi hizo na kwa sababu gani na zitatusaidia vipi kuongeza maarifa na kupunguza ujinga na pengine kutuwezesha kuvuta wawekezaji wa aina fulani?

Je, tunataka kuwa watu waaminifu na watenda haki au kuwa watu wasio na uaminifu na wanaobufu fedha tu wakati wote?

Je, tunaweza kuamua kuwa taifa linalojali usafi kuanzia chooni hadi Ikulu? Au ni taifa ambalo kampuni za wazoa taka ni za ndugu na shemeji wasio na uwezo wa kuendesha biashara hizo?

Je, tunataka tusifike kwa uchapaji kazi au kwa ulegevu na uvivu?


Je, tuanweza kuwa taifa linalojali wakati kama rasilimali isiyorudishika au watu wasiopenda kufungwa na wakati na mtu anaweza kuja kwenye kikao wakati wowote anaopenda?

Je, tunaweza kuwa taifa la watu wanaoheshimu ndoa na familia zao au la wazinzi na watumiaji kondomu maana tatizo sio zinaa ila ni ukimwi?

Je, tunataka kuwa taifa la watu wanaothamini elimu na maarifa au taifa la wababaishaji ambalo hata mawaziri na wabunge wanaishia kusoma magazeti ya Ijumaa, Uwazi na Kiu?

Je, tunataka kuwa taifa lenye aibu na haya au taifa la watu wasiokereka kuona watu wanatembea nusu uchi au hata uchi wa mnyama kabisa?

Je, tunataka kuwa taifa la watu ambao kiongozi asiyechangia maendeleo yao na ya nchi anabakia tu ofisini au taifa la watu ambalo mtu lazima aoneshe kustahili kubaki kwenye ofisi fulani?

Je, tunataka kuwa na nchi ambayo wizara zote zimekusnywa mahala pamoja dar es salaam na wala sio makao makuu ya nchi tarajiwa au nchi ya watu ambayo wizara zinajengwa kwenye mikoa au kanda ambazo huduma zake zinazohitjiaka zaidi?

Je, tuwe ni nchi inayotegemea misaada kwa maendeleo yake au tunaojua thamani ya rasilimali zetu na kuziuza kwa bei nzuri ili kiasi cha fedha za maendeleo zinazohitajika kila mwaka zipatikane kila siku?

Je, tuwe na nchi ambayo vyanzo vya mapato ya vyama vyake vya kisiasa ni siri au nchi ambayo kila shilingi chama cha kisiasa inayoipata inajulikana imetoka wapi?

Je, tuchanganye biashara na siasa au siasa iendeshwe na wanasiasa na biashara na wafanyabiashara?

Je, tuwe taifa la watu wanaokataa maovu na kutunuku mema au kinyume cha hivyo?

Je, tuwe taifa la watu waongo au watu wanaothamini ukweli mbele ya cheo au mali?


Haya ni baadhi ya maswali yanayopaswa tujiulize ili tuje na tamko la maadili ya kitaifa. Sio jambo la kuamuliwa siku moja na mtu moja bali linalohitaji mchakato ambao unashirikisha vyombo vyote vya habari, kulia na kushoto, ili hatima ya yote yapatikane aina ya maadili ambayo kila Mtanzania atajivunia kuwa ni maadili yake!


Vinginevyo nchi isiyo na maadili ina hatari ya vijana wake kuwa bendera fuata upepo. Vijana hao ambao wengi ni kama sponchi ni wepesi wa kunyonya hata mabaya, maovu na machavu na yanayotia kinyaa kama vile ni kitu cha kistaarabu, maendeleo na c ha kujivunia kumbe ni kinyume cha hivyo. Mwisho wa yote kijana anachanganyikiwa inakuwa ni hasara kwa familia na taifa!


Tuwaokoe watoto na kizazi cha nchi hii kwa KUWA NA KONGAMANO LA MAADILI YA KITAIFA litakalotoa TAMKO LA HAYA NDIO MAADILI YA MTANZANIA!

Friday, May 9, 2008

JMT: Njia muafaka za kurejesha imani ya wananchi kwa serikali

WENGINE wanaweza kuelezea mengi juu ya ni nini CCM ifanye ili iweze kurejesha tena imani ya wananchi kwa serikali yake. Lakini mimi leo napenda kuzungumzia mambo kama 15 tu hivi.



Kwanza, ni suala la Udhibiti wa daladala au usafiri wa umma katika miji ya Tanzania. Nilishawahi kusema na nitasema tena na kusema tena kuwa serikali ya Tanzania itakayofanikiwa kuwa na utawala bora itakuwa ni ile itakayoweza kudhibiti vilivyo usafiri wa umma jijini na mijini kwingineko Tanzania.



Kudhibiti ni pamoja na magari kuendeshwa kwa adabu na usataarabu unaostahili; kubeba abiria wanaoruhusiwa na si zaidi; na kuzingatiwa kwa kanuni zote za usalama barabarani.



Kutokana na uchache na ufinyu wa barabara lazima ufumbuzi haukuwa njia tatu bali mpangilio wa kazi za trafiki kiutaalamu zaidi kwa namna ambayo mabasi yanakuwa na vituo na siku maalumu za kukaguliwa na sio kusimamishwa ovyo barabarani.Isitoshe kwa magari ya watu binafsi kuwe na mpango wa magari yenye namba shufwaa kutembea siku moja na kupumzika siku moja. Na namba witri vivyo hivyo, lengo likiwa ni kupunguza wingi wa magari.


Na wakati huohuo kudhibiti idadi ya magari ambayo familia moja inaweza kuwa nayo.



Ninasema hivi kwa sababu daladala ni kielelezo cha jambo linalohusu takriban wakazi wote wa mji. Na utawala wake unaanzia ngazi ya Rais, Waziri husika, idara husika, wakuu wa mikoa, wakuu wa polisi, wakuu wa usalama barabarani na askari walioko barabarani.



Kama utawala unafanya kazi ipasavyo toka juu hadi chini basi adabu, ustaarabu ha heshima katika usafiri wa umma vitakuwepo. Kama utawala ni legelege hili kamwe halitawezekana. Na hili litakuwa ni kielelezo kamilifu cha jinsi Wizara nyingine nazo zinavyofanya kazi katika nchi hii.



Pili, katika miaka hii ya kompyuta na mtandao ni rahisi kwa Rais na Mawaziri wake kudhibiti fedha hazina na wizarani kama vile mchezo.



Lakini kama wanasiasa wana lao na hawapo kwa ajili ya maslahi ya nchi na watu wake bali kwa ajili ya chama fulani basi hili nalo litakuwa muhali. Maana kukosa udhibiti katika jambo lolote ni ishara wazi kuwa wahusika hawataki udhibiti ili waweze kufanya madudu yao na iwe ni vigumu kukamata wahusika.



Fedha zilizopo hazina lazima zilindwe na kutumika katika kuwapa nafuu Watanzania kwa kila hali na kuongeza ubora wa maisha yao kila kukichwa na sio vinginevyo.



Jambo la tatu ambalo tunaweza kuishauri serikali ni kuhakikisha kwamba kodi na tozo ambazo ni kero kwa wananchi zinaondolewa.



Kwa mfano, usumbufu na ucheleweshaji unaotokea katika vituo vya mabasi vya mikoani na vituo vya daladala unaletwa na tozo la kero la kila siku kwa wenye mabasi.



Lakini ni dhahiri kuwa mabasi ya mkoani yanaweza kutozwa kodi kupitia tiketi zao ambapo wenye mabasi wataitunza kodi hiyo kama 'withdrwal taxes' na kisha kuilipa baadaye kwa serikali.



Aidha wenye daladala wanaweza kuwekewa kodi fulani na jiji wakati wa kulipia ushuru au kodi za magari na hiyo ikawa sawa na matozo ya usumbufu kwa kulipishwa daladala kila zikiingia au kutoka kwenye vituo fulani fulani vya mabasi.



Kuna sehemu nyingine kama hospitali, sokoni, viwanja vya maonesho, viwanja vya ndege, stesheni za treni na kadhalika ambapo kwa kweli kodi na tozo zilizopo ni kero zaidi na dalili ya jinsi serikali yetu ilivyo nyuma katika kuwaondolea wananchi usumbufu usio wa lazima katika maisha yao ya kila siku. Hili linakuwa na uzito wa ziada pale ukiangalia jinsi wananchi wanavyokabiliwa na ugumu wa maisha hivi sasa.



Dalili ya tano kuwa serikali itaweza kurudisha imani ya wananchi ni kuonesha kuwa haikuwa 'serious' wakati ilipobuni mradi wa kuleta mvua kwa kupiga mabomu mawingu na badala yake itangaze mkakati wa uvunaji maji ya mvua katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Dar es salaam.



Mvua za hivi karibuni zimetutia Watanzania aibu na hasa sisi wa Dar es salaam. Kisa, bahari iko pua na mdomo lakini kuna maji yalijaa barabara fulani kiasi cha kutisha na bahati yao wakubwa siku hiyo maana hakuna aliyekuwa akienda au kutoka 'eyapoti'.



Lakini hiki ni kichekesho cha mwaka maana maji hayo ya mvua yangevunwa sehemu kama Tabata na Ukonga zingelipata maji ya kutosha kwa sehemu yote ya mwaka iliyobakia baada ya mvua kwisha.



Jambo la sita ni Kuwepo kwa barabara safi ili kufikisha sokoni mazao ya wananchi. Kuna sehemu mbalimbali ambazo leo zina mahindi, mpunga, maharagwe na mboga za kila aina lakini kutokana na ugumu wa usafiri watu hao wanashindwa kuuza walichovuna kwa bei nzuri na wanaendelea kubaki katika lindi la umasikini mkubwa. Je, watu kama hawa si ujinga tu ndio utakaowafanya wawe na imani na serikali iliyopo?



Kuna watu wanaodai kuwa migodi ya madini ikiwepo ile ya dhahabu, tanzanite, almasi na vito inaweza kabisa kutozwa kodi itakayotosha kulipia tiba na elimu Tanzania. Na hivyo wananchi masikini wasiwe na ulazima wa kulipia huduma hizo muhimu na zisizokwepeka.



Hili likifanyika serikali itakuwa na njia ya sita ya kurudisha imani ya wananchi kwa uongozi na usimamizi wake wa masuala ya kiuchumi na kijamii.



Saba, ingawa halikusikika lolote juu ya kipato cha wananchi lakini ni dhahiri kuna pengo kubwa kati ya matumizi na mapato ya wananchi. Serikali inayotaka kupata imani ya wananchi wake ni lazima ihakikishe kuwa wananchi wake wana kipato kinachotosheleza mahitaji yao ya msingi.



Machiavelli alishawahi kumwambia bin Mfalme mmoja kwamba ili aweze kutawala raha mustarehe ni lazima ahakikishe kwamba wananchi wake hawalali na njaa. La sivyo awe tayari kwa lolote litakalotokea.



Nane, sambamba na suala la kipato ni jinsi ya kupunguza matumizi ya wananchi kwa Kuwa nishati mbadala na nafuu kwa wananchi. Kilichopo sasa hivi ni porojo na gumzo la gesi, mkaa wa mawe, nishati ya jua na kadhalika lakini haionekani kama serikali ina nia ya kufanya nishati hii ipatikane kwa wingi na kwa urahisi kwa wananchi wote.



Suala la nishati ni bomu linalongojea kulipuka wakati wowote toka sasa kama serikali isipoanza kwa dhati kujiingiza katika kutafuta njia za kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala ya gharama nafuu.



Hata kwa kipofu ni dhahiri kuwa hivi sasa biashara kati ya Tanzania na nchi za Kiarabu na mashariki ya mbali inakuwa kwa kasi sana. Njia ya tisa ya kurejesha imani ya wananchi kwa serikali ni kuchochea na kurahisisha biashara na nchi za Imarati na Mashariki ya Mbali kwa faida ya Watanzania na nchi jirani.



Tusidanganye kuwa kilimo ni uti wa mgongo Tanzania. Sio leo. Ni kesho. Leo ni vyema tukamate biashara sawasawa ili tuweze kudunduliza na baadaye kuwa na mitaji kwa ajili ya kilimo na viwanda. Vinginevyo, tunajidanganya.



Hili linaweza kufanyika kwa Tanzania kuwa na ndege kadhaa za mizigo zitakazobeba mizigo toka Uarabuni na China na kisha kuipakua Dar es salaam, Kigoma, Tunduma, Ngara, Namanga na Mbamba Bay kwa ajili ya kuhakikisha wafanyabiashara wa Tanzania wanaingia mpaka nchi zisizo na bahari kufanya biashara ya faida kubwa zaidi huko.



Kumi, ikumbukwe kuwa mali zote za umma-ikiwemo viwanda, makampuni au mashirika, nyumba na kadhalika vilitokana na fedha za kila Mtanzania. Iweje dhuluma ya wazi ifanyike kwa watu fulani fulani tu kujibinafsishia na kubinafsishia wageni na sisi wengine wote tutoke patupu. Lazima pawe na suala la kuwafidia Watanzania kutokana na ubinafsishwaji wa mali zao uliofanywa kinyemela na kiupendeleo na kidhulumati.



Kama serikali italifanya hili yenyewe bila kungojea shinikizo la wanaharakati wa kulia au kushoto basi serikali itauwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kurejesha tena imani ya wananchi.



Ikumbukwe hivi sasa Marekani na Uingereza zina mikakati ya kuwarudishia pesa watu wao baada ya kugundua dhuluma inayofanana na hiyo ilifanyika huko.



Suala la kumi na moja ni kuhakikisha kuwa wawekezaji wote wachovu wananyang'anywa kile walichopewa kukiendesha na badala yake wanapewa wawekezaji wenye uwezo na ari ya kuichangamsha nchi kiuchumi, kijamii na kibiashara.



Iweje tuwape makampuni machovu ambao wawekezaji wake wanategemea kujitajirisha kwa mtaji wetu wenyewe badala ya kujitajirisha kutokana na uwekezaji wao?



La kumi na mbili ni suala la kuwachukulia hatua wala rushwa papa na kuacha kutudanganya kwa kuvinasa vidagaa hapa na pale.



Na hili nalo sio la maneno bali vitendo. Muda wa porojo na ahadi za kitoto sasa umepita. Vinginevyo tuwaambie watu wetu kwamba mtu mzima hatishiwi 'nyau'!



Kumi na tatu, umefika wakati wa kuipa mikoa uhuru wa kujiendesha yenyewe na kuwa na uwezo sio tu wa kuchagua kiongozi wao wa mkoa bali pia kwa mkoa huo kutawaliwa na chama chenye wabunge wengi. Hili linafanyika India, Ujerumani, Uingereza, Marekani na kadhalika na ndiko tunakotakiwa kwenda na sio vinginevyo.



Kubwa, hata hivyo ni kuwa kitendo chochote kinachowaongezea wananchi uwezo wa kusimamia na kuendesha mambo yao kwa ufanisi na ufanifu zaidi ni kitendo cha maendeleo. Madaraka mikoani yalizaliwa yakafizwa na chama tawala lakini imefika wakati kwa Watanzania waona mbali na mbele kuhakikisha hili linafufuliwa kwa sababu tumegundua kuwa hatuna watu wenye uwezo wa kuiendesha vyema mikoa 26 kwa mpigo.



Mikoa inayojiendesha yenyewe itarahisisha masuala ya uwekezaji, ujenzi wa miundo mbinu, kukuza kipato cha watu wake, kuboresha huduma za jamii kwa kiwango wanachokitaka na kwa kila hali kukuza uchumi wao kwa haraka zaidi kuliko inavyoweza kufanyika ikiwa kwapani kwa serikali kuu.



Hofu ya kuwa madaaraka mikoani au serikali za mikoa au majimbo zitaondoa amani na mshikamano wetu zimepitwa na wakati. Hatari kubwa tuliyonayo leo ni kuwa ukiritimba wa madaraka na uongozi toka Dar es salaam na wala sio Dodoma sasa unatuletea mchecheto, mdebwedo na utapiamlo wa Kimaendeleo.



Aina ya viongozi tulionao inaonekana hawana ubavu wa kusimamia mikoa ishirini na ushee kwa mpigo.


Mikoa mingi inageuka mayatima ambao wanakumbukwa mara moja tu baada ya kila miaka mitano.


Tuna hatari zaidi ya kukosa amani na mshikamano kwa watu wachache Dar es salaam kung'ang'ania mambo yote ilhali tunajua fika uwezo wa kutekeleza hata mojayakumi ya matatizo ya mkoa husika hawana.



Suala la kumi na nne ni kuzipa dini uhuru wa kujiendesha ikiwemo na kuruhusu mahakama ya Kadhi kwa Waislamu.



Kama wakatoliki na waludherani wana mifumo yao ya kumaliza matatizo ya waumini wao ndani ya kuta za makanisa yao ni muhimu pia kwa Waislamu kuwa na taasisi na uongozi ulio huru na sio vibarakala wa serikali kwa faida za umoja na amani miongoni mwa waumini wa dini hiyo.



Na ikumbukwe ahadi ni deni. Na kama kweli serikali ya sasa inataka kurejesha imani ya Waislamu kwa viongozi wake ni muhimu ahadi hii ikatekelezwa sasa bila kuchelewa.



Kumi na nne ni kuhakikisha wizara zote zinakuwa kwenye ghorofa moja pale Dodoma na Dodoma inakuwa kweli makao makuu ya nchi.

Hili halina mjadala na mzungu wa kula hafundishwi mwana.


Ninategemea hata hivyo wizara mpya huko Dodoma hazitakuwa sitini au hata thelathini bali kati ya 12 na 18 tu. Nina hakika tuna wizara nyingi ambazo zinastahili kuwa wakala au idara zinazojitegemea ya hili au lile, jambo litakaloruhusu pia matumizi bora ya rasilimali watu na tathmini kazi zinazofanya kazi barabara!


Wingi si hoja. Hoja ubora.



***