Thursday, July 15, 2010

Mahakama ya Rufaa imethibitisha Katiba Mpya yahitajika ...

WAKATI wananchi wa Kenya karibuni watapigia kura pendekezo la Katiba mpya nchini mwao, Tanzania, nchi iliyoitangulia Kenya katika kukubali demokrasia ya kisiasa haijaona umuhimu wa kuwa na katiba mpya licha ya mapungufu mengi ambayo watu wengi nikiwemo na mimi tumekwishaonesha mapungufu yake kadhaa. Kwa kifupi katiba tuliyo nayo haitofautiani na kutumia taipureta katika karne ya kompyuta.

Hata hivyo, masuala kadhaa yaliyozuka ndani na nje ya nchi kwa hivi sasa yanaashiria kuonesha kuwa kukataa katiba mpya nchini Tanzania ni jambo ambalo linakaribia kupoteza sababu na mantiki katika kila nyanja ya maisha, siasa na kazi.

Mathalani, kadhia ya mgombea huru na jinsi mhimili wa sheria ulivyoterereka na kukwepa wajibu wake umeonesha wazi kwamba bila ya kuwa na katiba mpya jambo hili litafanywa kwa mizengwe na matakwa ya chama tawala na sio kisheria wala kidemokrasia. Hii ni kusema ipo hatari kubwa ya nchi kuendelea kuongozwa kutokana na haja na matakwa ya mtu au watu badala ya kuwa na mifumo hai inayofanya kazi bila kuingiliwa na utashi wa mtu katika maeneo mbalimbali ya utawala na uongozi wa nchi.

Katiba iliyopo sasa inakubali na kuamini katika uhuru usiokuwa na kikomo ndani ya sheria za nchi. Wanachokitaka wengine ni kuweka mipaka kwa uhuru wa Mtanzania, hususan ule wa kuchagua na kuchaguliwa ndani au nje ya chama cha kisiasa.

Tukio lingine ni lile la kupitishwa kwa itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki. Inaelekea Tanzania imekutwa katika hali ya kuwa bado imeshusha kaptula yake na inataka faragha ya muda kujiweka sawa. Badala ya mambo haya, hata kufanyika kwa msaada wa ushauri na utafiti wa wasomi wetu, wataalamu na mabingwa wa nyanja mbalimbali, inaelekea yanafanyika bado kisiasa na matakwa ya watu fulani ikidhihirisha kuwa hata tukipewa miaka 20 hatutaweza kubadili chochote. Kusahihisha jambo hili ni lazima pawe na katiba mpya na itakayobainisha waziwazi ni kwa kiasi gani nchi hii itatoa ruhusa ya kumegua uhuru wake katika kutafuta umoja wa Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla. Ni lazima tuwe na katiba inayoona mbali kwa miaka hata zaidi ya hamsini. Sio katiba iliyoishia katika uhuru na Azimio la Arusha.

Kuna wanaoamini kwamba Tanzania haiwezi kuendelea kama kila kitu kitakuwa kinaamuliwa kutoka Dar es salaam. Jamaa hao wanaamini ipo haja ya kuwa na mikoa huru kiuchumi na kijamii kama tunataka kuendelea kwa uhakika na haraka zaidi. Tishio kwa umoja kupitia ukabila hivi sasa sio kubwa kama tishio la ukabila wa kichama. Je, uziro wa jambo hili haulifanyi kuwa katika katiba mpya ?

Wakati Zanzibar ina mahakama ya Kadhi kama ilivyo kwa Kenya na Uganda na suala hili limo katika Katiba ya nchi zao na ambazo ukitoa Zanzibar ni nchi zenye wakiristo wengi zaidi kuliko Waislamu chama tawala hapa nchini kimefikia uamuzi wa kukataa mahakama ya kadhi isiwemo katika katiba kinyemela. Jambo linaloacha ufa wa kutisha siku zijazo za Waislamu wenye siasa kali kwenda njia nzima na kuwa na shariya maana hawakujumlishwa na usaikula eti kwa kisingizio cha kuogopa gharama ambazo zinatumika kwa wananchi wale wale wanaochangia hazina ya taifa kwa kodi na matumizi yao mbalimbali. Uamuzi huu unakuwa sio tu undumilakuwili bali pia ni wenye kuning'inia kwa kamba ya shinikizo za nje na hauashirii mahusiano mema kati ya imani zetu za kidini katika miaka ijayo. Hili sio jambo la kutania, na watu wachache kwa shinikizo yoyote ile isikubaliwe wafikie maamuzi ambayo kizazi cha baadaye kitakuja kuyajutia. Ni lazima suala hili litambulike kikatiba na sio vinginivyo.

Sehemu kubwa ya Waislamu hawaitambui BAKWATA, lakini kwa sababu moja au nyingine serikali bado inashinikiza kuwa BAKWATA peke yake ndio mwakilishi halali wa Waislamu. Hii sio bishara njema, ni lazima pawepo na katiba mpya ili kudhihirisha wazi uhuru wa kila dini kujiundia wenyewe vyombo vya kuwawakilisha katika masuala mbalimbali. Taasisi inayoonekana kufadhiliwa na kulindwa na serikali haiwezi kukubalika kuwa mwakilishi halali wa wanaimani wanaohusika.


Kuna wanaoamini kwamba vyombo vya habari vya serikali ni mzigo kwa walipa kodi usio wa lazima, j e, hili halioneshi kwamba ipo haja ya katiba mpya ambayo pamoja na mambo mengine itaangalia pia
nini uwe uhusiano wa vyombo vya habari, na serikali; vyombo hivyo na vyama vya siasa na vyombo hivyo na wananchi ? Kwa wengi, vyombo hivi kama vilivyo vingi vinginevyo vinaonekana ni mianya kwa baadhi ya watu na taasisi kula fedha za umma bila ya wachungaji kupiga mayowe na wakati mwingine bila kujua.

Dai mojawapo kubwa la vyama mbadala nchini ni kuwepo kwa tume huru. Tume itakayokuwa haiegemei upande wowote na hivyo kusimamia chaguzi zitakazokuwa huru. Je, ni kwa kiasi gani hili linaweza kukamilika bila ya kuwa na katiba mpya ?

Toka tupate uhuru azma moja yetu kubwa ilikuwa ni kupunguza tofauti kati ya miji na vijiji, wakulima na wafanyakazi, matajiri na maskini je, hili, limefanikiwa kwa kiasi gani. Hivi 'apartheid kati ya miji na vijiji' inaweza kuondoka bila ya kuwepo kwa katiba mpya ?

Kuna watu wa makabila mbalimbali nchini ambao wanaamini kwamba redio zingelikuwa zinatangaza kwa lugha za makabila yao basi sio tu wangelihabarika, kuelimika na kustareheka zaidi lakini mapambano yao ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yangelikuwa rahisi zaidi. Lakini sheria na katiba iliyopo havielekei kuoana katika kauli za kama iwepo au isiwepo ruhusa. Isitoshe wanasiasa wa kale lakini wasiothamini utu na utamaduni wetu hawalikubali hili. Wanaleta hofu ya bure ambayo inastahili sasa kuwa dhidi ya wanasiasa wenye ubaguzi wa kichama nchini. Nchi kwa hiyo inatawaliwa kwa uoga badala ya hoja za msingi zenye mantiki inayokubalika.

Habari za mama na mabinti wetu kujifungua barabarani na chini ya miti haziachi kusikika toka huku na kule. Madaktari na manesi wetu wanalaumiwa kwa roho mbaya lakini hili linaanzia kwenye mishahara mibaya. Je, bado kweli hatujaona haja ya kuwa na kipengele ndani ya katiba mpya kinachozungumzia kwa kina ni nini iwe sera ya afya kwa wananchi wetu-wenye nacho na wasio nacho daima dawamu ? Haisemi lolote jinsi ya kuboresha hospitali hizo ili ziweze kutibu wanaopelekwa nje kutibiwa na vilevile kutibu wagonjwa kutoka nje na nafuu inayopatikana iwe ni nafuu itakayoweza kutoa tiba ya bure kwa watu masikini.

Kuna suala la usafi, mipango miji na utunzaji mazingira mijini na vijijini ambalo hata hapa Dar es salaam wanapoishi wakubwa linaelekea sio tu halina mwenyewe bali hakuna viwango vya kumzawadia mtu zabuni ya kusafisha mji na matokeo ya hili ni kuwa msafisha mji na vyombo wanalitia jiji uchafu na sura mbaya zaidi, je, halistahili nalo kusahihishwa na katiba mpya ? Na katiba hiyo haiwezi kwenda mbali na kutangaza rasmi maadili ya Watanzania kama yatakavyokubalika na walio wengi.
Suala la madini nigodi pamoja na kuwepo na sera mpya bado linastahili kuingizwa ndani ya katiba kwa namna ambayo watu na madini yetu yataonekana kuwa na thamani zaidi kuliko wawekezaji na mitambo yao na vizawadi vya barabara, shule na zahanati wanavyotudanganya navyo. Zanzibar inadai mafuta ni yake wakubwa bara wanasema mafuta ni yetu. Tumfuate nani? Dawa hapa hivi kweli siyo katiba iliyo wazi juu ya jambo hili ?

Kuna wanaoamini kuwa mashirika kama yale ya hifadhi za jamii yanastahili kwa kiasi kikubwa kumilikiwa na wanachama wenyewe na sio na serikali na wanasiasa. Wanadai umilikaji wa sasa hivi unawanyonya na kuwapunja wanachama kwa njia nyingi. Makato ya mwanachama yakigeuzwa ni hisa ndani ya mashirika hayo wanachama watafaidika zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. La, sivyo, basi pawe na uhuru wa kuanzisha hifadhi huru za jamii kwa kila tarafu.

Kuna wanaoamini, Tanzania yenye viongozi wanaotaka kweli kuwaondoa wananchi wake toka kwenye umaskini ina uwezo kwa kutumia rasilimali zake yenyewe kujengea kila familia nchini, mjini na vijijini angalau nyumba ya vyumba viwili. Jambo hili sio tu litazusha ajira kubwa na pato kubwa kwa nchi na watu wake bali pia litaondosha aibu ya kila Mtanzania kuwa na mradi wa kujenga nyumba ya kuishi badala ya kujenga biashara au kiwanda.

No comments: